MWALIMU NYERERE KAMA NILIVYOMFAHAMU MIMI.
Maelezo yanayotolewa hapa kuhusu Mwalimu Nyerere, yanatoka kwangu mimi binafsi. Yanatokana na vile nilivyomfahamu kiongozi huyo nilipokuwa ninafanya naye kazi karibu sana kwa muda mrefu wa miaka ishirini na mitano, nikiwa msaidizi wake wa karibu.
        Kabla ya kueleza sifa za Mwalimu Nyerere, ni vizuri kwanza kumkumbusha msomaji kwamba, mwalimu nyerere alikuwa ni binadamu kama walivyo binadamu wengine. Kwa hiyo bila shaka yeye pia alikuwa na mapungufu yale ya binadamu, kama vile hasira, amabazo kwa wakati mwingine zilimsababishia kufanya makossa katika uamuzi wake kutokana na hasira iliyompata ghafla. Ipo mifano kadhaa ya kuthibitisha hilo.

Mifano ya uamuzi wake uliotokana na hasira
Mfano mmoja ni ile siku alipowavurumisha wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam waliofanya maandamano ya kupinga mpango wa wanafunzi waliomaliza elimu ya Sekondari kulazimika kwenda kwenye mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT). Katika tukio hilo, baadhi yao walipayuka maneno ya ovyo kwa kusema “Heri wakati wa ukoloni” wakimaanisha kwamba hali ya nchi ilikuwa bora Zaidi wakati wa utawala wa Kikoloni. Maneno hayo yalimkasirisha Rais Nyerere kiasi cha kuamuru kuwafukuza Chuoni  na kuamuru Chuo hicho kifungwe, wanafunzi wote walirudishwa makwao kwa likizo ya lazima ya miaka miwili, ili watumie muda huo kutafakari kosa waliolifanya wakiwa pamoja na wazazi wao.
         Mfano mwingine unaofanana na huo, ni wakati wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam walipofanya maandamano ya kupinga tukio la kulaani Sertikali ya Uingereza, wakati koloni lake la Rhodesia ya Kusini lilipojitangazia uhuru wake kinyemela mwezi Novemba 1965; na serikali ya Uingereza haikuchukua hatua yoyote dhidi ya viongozi waasi wa koloni hilo.
         Maandamano hayo yaliwafikisha kwenye jengo la Ubalozi wa Uingereza mjini Dar Es Salaam, ambapo waliharibu baadhi ya mali zilizokuwemo katika jengo hilo. Kutokana na kitendo hicho, vijana waliohusika walikamatwa na polisi na kuzuiliwa katika kituo Kikuu cha Polisi. Baada ya hapo, Mwalimu Nyerere aliagiza vijana hao wapelekwe Ikulu ili azungumze nao. Walipofika huko, aliwapokea vizuri na kuwaeleza ubaya wa kosa lao la kufanya maandamano bila kibali cha Polisi; pamoja na kosa jingine la kuharibu mali katika jengo la Ubalozi wa Uingereza.
Hatimaye aliwataka waende kuomba radhi kwa Balozi wa Uingereza kwa kosa hilo la kuharibu mali ya Ubalozi huo. Baada ya kusema hivyo, Rais Nyerere aliuliza kama kulikuwa na yeyote miongoni  mwao ambaye alikuwa anapinga wazo hillo la kwenda kuomba radhi. Mwanafunzi mmoja akajitokeza na kusema kuwa yeye analipinga. Papo hapo Rais Nyerere alimwamuru kamishina wa polisi amkamate kijana huyo na kumpeleka akachapwe viboko sita. Siku moja baada ya tukio hilo; Rais Nyerere alimwita kijana huyo aende Ikulu, ambapo alimweleza kwamba alikuwa ametoa adhabu hiyo kutokana na hasira iliyompanda ghafla, na kwamba hasira hiyo ilimrejesha kwenye hulka za ualimu wake wa darasani, ambapo wanafunzi hupewa adhabu za kuchapwa viboko. Kitendo hicho kinadhihirisha uungwana wa Mwalimu Nyerere alidhihirisha kuwa tayari kukiri kosa, bila kujali wadhifa mzito aliokuwa nao kama Raisi wa Nchi.
           Mfano mwingine ni pale alipomfukuza kazi ghafla aliyekuwa Waziri wa Fedha wakati huo. Hii ilitokana na waziri huyo kushindwa kutekeleza maagizo ya Rais ya kukataa shinikizo la kushusha thamani ya shilingi ya Tanzania; ambalo lilitolewa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) mwanzoni mwa mwaka 1981. Kilichotokea kwa Waziri huyo ni kwamba badala ya kutekeleza maagizo ya Rais, Yeye aliunga mkono shinikizo la IMF kwa kushabikia kushushwa kwa thamani ya shilingi ya Tanzania. Rais Nyerere alikasirika sana alipopata habari hizo. Alimwita Waziri huyo na kumtaka awasilishe kwake mara moja barua ya kujiuzulu wadhifa wa Waziri wa Fedha.
             Mfano mwingine ni siku alipoulizwa maswali ya kipuuzi na mwandishi mmoja wa habari wa Kenya, swali ambalo lilimpandisha hasira. Waandishi wa habari wa Kenya, walikuwa wamesikia maneno yaliyosemwa na mwanasiasa uchwara mmoja wa Tanzania, aliyelopoka kwamba eti  Mwalimu Nyerere hakuwa Mtanzania wa kuzaliwa hapa, bali ni mtu aliyetoka Burundi. Upuuzi huo uliandikwa kwenye baadhi ya magazeti ya hapa nchini. Siku moja baadaye, Mwalimu Nyerere akiwa katika safari zake za kawaida, alipita katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, Nairobi. Mwandishi mmoja wa habari wa Kenya aliyekuwepo hapo uwanjani akamuuliza Mwalimu Nyerere swali, “Mwalimu , tumesikia tuhuma kuwa wewe siyo Mtanzania, bali ni Mrundi. Je, tuhuma hizo zina ukweli?” swali hilo lilimuudhi sana Mwalimu Nyerere, akamjibu kwa hasira na kejeli, “Umesema kuwa umesikia tuhuma hizo. Je, ukisikia tuhuma nyingine kwmba mimi ndiye baba yako niliyezaa na mama yako, utakuja kuniuliza kama tuhuma hiuzo ni kweli?”Jibu hilo liliwafanya waandishi wenzake wote  watambue kwamba swali la mwenzao huyo lilikuwa la kijinga na halikustahili kuulizwa, kwani jibu lake lilikuwa wazi kabisa kuwa siyo kweli.




SIFA ZA MWALIMU NYERERE
Ukiondoa mapungufu ya aina hiyo ambayo ni ya ;kila binadamu, mwonekano wa jumla wa tabia ya Mwalimu Nyerere kwa watu mbalimbali, ulikuwa ni wa kuheshimika sana, hususani katika maeneo yafuatayo:

Alikuwa na ujasiri wa kukiri makosa aliyoyafanya
Hapo juu tumetaja mfano mmojawapo wa sifa yake hii. Yaani sifa ya kuwa na ujasiri, pamoja na unyenyekevu wa kukiri makosa ambayo alifanya katika uongozi wake. Si viongozi wengi duniani walio na ujasiri wa aina hiyo.
           Kuna mifano mingine miwili ambayo inadhihirisha sifa yake hii. Kwanza, ni uamuzi wa kufuta Serikali za Mitaa mnamo mwaka 1975. Kama tutakavyoona baadaye, yeye mwnyewe baadaye alitoa kauli bungeni, ya kukiri kosa hilo. Alisema hivi: ‘kufikia mwaka 1982, tukatambua kwamba tulifanya kosa kubwa kwa kufuta Serikali za Mitaa. Kwa hiyo, tukaliomba Bunge kupitisha sheria ya kuzizindua tena wilayani na mijini”. Kosa la pili alilokiri ni kufutwa kwa vyama vya ushirika. Katika kukiri kosa hilo, Mwalimu Nyerere alisema “Vyama vya Ushirika vimeanzishwa tena. Kufutwa kwa vyama hivyo lilikuwa kosa jingine kubwa tulilolifanya katika miaka iliyopita”. 

Alitumia elimu yake kwa faida ya wote
Sifa yake nyingine ni kwamba Mwalimu Nyerere alitumia elimu yake vizuri sana kulingana na ahadi ya mwanachama wa CCM, inayosema kuwa “Nitajielimisha kwa kadri ya uwezo wangu, na nitatumia elimu yangu kwa faida ya wote”.
            Kwa hakika Mwalimu Nyerere alitumia elimu yake kwa faida ya wote. Kila hotuba aliyoitoa, ilikuwa ni darasa tosha kwa wasikilizaji wake. Aidha, Makala zake nyingi na za aina mbalimbali alizoziandika, vilevile zilitosha  kabisa kuwa ni Makala za kufundishia.
              Kwa bahati nzuri, hotuba zake nyingi zimechapishwa kwenye vitabu vyake vyenye majina ya : Uhuru na Umoja; Uhuru na Ujamaa; pamoja na vitabu vingine vingi alivyoviandika yeye mwenyewe, kama vile  vya Uongozi wetu na Hatima ya Tanzania 
               Pia, Mwalimu Nyerere alikuwa na kipaji maalumu cha kubuni vidokezo vinavyoeleza  jambo kubwa katika maneno machache . mifano yake ni kama vile , “Uhuru na Kazi” ; “Inawezekana, timiza wajibu wako” ; “We must run while others walk” (Sisi lazima tukimbie wakati wenzetu wanatembea);  “Linalowezekana leo, lisingoje kesho”; “Kupanga ni kuchagua” n.k

Alikuwa na kipaji cha kufundisha kwa kutumia mifano na methali
Kwa mfano, katika moja ya hotuba zake za mwanzo baada ya kuzaliwa kwa CCM, Mwalimu Nyerere alizungumzia suala lililokuwa linamkera sana, la uchafu unaosababishwa na takataka nyingi zinazotupwa ovyo katika mitaa yetu. Katika kuwatahadharisha wananchi wasipuuzie kuwepo kwa tatizo hilo, kwani linaweza kuleta mlipuko wa magonjwa; alitumia methali ya Kizanaki, ambayo tafasiri yake ni, “Mfichaficha maradhi, kilio kitamuumbua”.
              Aidha katika utaratibu wake wa kusimamia maadili ya viongozi, mara nyingi alitumia methali hii, “Mtoto akichezea wembe, utamkata papo hapo”. Akimaanisha kwamba, Kiongozi anayekiuka maadili sharti achukuliwe hatua mara moja, bila kumchelewesha.
Siku moja, Mwalimu Nyerere alipokuwa akisisitiza umuhimu wa mafunzo kwa viongozi na watendaji wa Chama cha Mapinduzi, aliamua kutumia hadithi ya mtoto wa jongoo, ambayo aliihadithia mwenyewe kama ifuatavyo:
“Mama jongoo alizaa mtoto. Mtoto huyo alipojikuta ana miguu mingi sana, akamuuliza mamaye; Je, mama, katika miguu yote hii, nikitaka kutembea nitangulize mguu gani? Mama jongoo akamjibu: wewe tembea tu, miguu itajua yenyewe itakavyojipanga”.
Alikuwa akizungumzia umuhimu wa kuandaa mafunzo ya mara kwa mara kwa ajili ya viongozi na watendaji wa chama chetu. Alisema kuwa mahitaji ya mafunzo kwao hayawezi kupewa majibu kama hayo ya mama jongoo; kwamba eti wakisha chaguliwa au kuteuliwa, tuwaambie tu. “fanyeni kazi mliyopewa. Jinsi mtakavyofanya mtajua wenyewe” (Mtajiju). Alituasa kuwa “Hiyo haifai kabisa”.
Katika utaratibu wake huo wa kufundisha kwa kutumia mifano, alipochukua hatua ya kumwajibisha kiongozi kwa kosa ambalo angependa liwe ni mfano kwa viongozi wengine wote, aliwapelekea taarifa juu ya hatua aliyokuwa amemchukulia kiongozi aliyemwajibisha ili wajue.
Siku moja katika miezi  ya mwanzo yam waka 1981, Mwalimu Nyerere alikuwa katika ziara mkoani Mwanza. Kulikuwa na tukio moja la kujaribu kumdanganya, ambalo lilisababisha Mkuu wa Mkoa achukuliwe hatua ya kufutwa kazi. Mkuu huyo wa Mkoa alimpeleka Rais Nyerere kumwonesha shamba la mbogamboga, ambalo alidai kuwa ni shamba la Ujamaa, kwa madhumuni ya kumthibitishia Rais kuwa alikuwa msitari wa mbele katika kutekeleza Azimio la Arusha.
             Inasemekana kuwa Mwalimu Nyerere alidokezwa mapema na wasaidizi wake, kwamba shamba hilo lilikuwa limepandwa usiku wa kuamukia siku hiyo ya ziara yake, kwa madhumuni ya kumdanganya Rais. Kwa hiyo alipofika hapo shambani, alishika mmea mmojawapo na kuutikisa ili kuona uimara wake. Mmea huo uling’oka, kwa kuwa mizizi ilikuwa bado haijashika vizuri.
              Aliporejea Ikulu baada ya ziara hiyo, Rais Nyerere aliandika barua ya kumfukuza kazi mara moja Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, ili kumwajibisha kwa kosa hilo kubwa alilokuwa amelifanya. Lakini Rais Nyerere hakuishia hapo, bali aliandika maelezo marefu ya kufafanua kwanini alichukua hatua hiyo; na aliagiza maelezo hayo yakapelekwa kwa wakuu wote wa Mikoa yote, ili liwe ni fundisho kwao.
              Mfano  mwingine ni mwaka 1977, Rais Nyerere alipowawajibisha mawaziri wawili wa Serikali yake na Wakuu wa Mikoa wawili, kwa kuwataka waandike barua mara moja za kujiuzulu nafasi zao za uongozi walizokuwa nazo. 
Sababu yake ya kuwachukulia hatua hiyo ilikuiwa ni kuwawajibisha kutokana na mauuaji yaliyokuwa yamefanywa na vyombo vya usalama vya Serikali katika mikoa ya Shinyanga na Mwanza. Mawaziri wawili waliowajibishwa ni Waziri wa mambo ya Ndani ya Nchi, wakati huo akiwa ndugu Ali Hassan Mwinyi pamoja na Waziri mwenye dhamana ya Usalama wa Taifa. Wakuu wa Mikoa waliohusika ni wa Mikoa ya Shinyanga na Mwanza.
Kwa hiyo, aliagiza nakala za barua hiyo wapelekewe viongozi wote wa Serikali, hususan Mawaziri na Wakuu wote wa Mikoa na Wilaya, ili suala hili la Kiongozi kuwajibika kwa makosa yaliyofanywa na watendaji walio chini ya dhamana yake ya uongozi, liwe fundisho kwao, na wajifunze kuiga mfano huo wa ndugu Ali Hassan Mwinyi.

Alihamasisha watu kwa kutumia “nguvu ya hoja”
Mwalimu Nyerere alikuwa na uwezo mkubwa sana wa kuridhisha watu kwa kutumia nguvu ya hoja zake. Kwa kingereza uwezo huo unaitwa “power of persuasion”. Uwezo huo ndio uliomuwezesha kupata mafanikio makubwa katika malengo yake mengi ya kisiasa; kama inavyodhihirishwa na matukio yafuatayo:
               Kwanza, ni pale alipofanikiwa kuwaridhisha kwa nguvu za hoja  zake, wanachama wa iliyokuwa asasi ya kupigania maslahi ya wafanyakazi wa Kiafrika katika Serikali ya Kikoloni, iliyokuwa inaitwa “Tanganyika African Association” (TAA). Alifanikiwa kuwashawishi wanachama wa asasi hiyo kukubali wenyewe kuvunja chama chao hicho, na badala yake kuunda chama kipya cha siasa cha “Tanganyika African National Union” (TANU), mnamo mwezi Julai, 1954, ili kiwe ni chombo cha kisiasa cha kupigania Uhuru wa Tanganyika.
            Mfano wa pili ni pale alipofanikiwa kuwaridhisha kwa kutumia nguvu ya hoja zake, wanachama wa chama hicho cha TANU, wakakubali kukivunja chama chao hicho  na kukiunganisha na chama cha Afro-Shirazi Party (ASP) cha Zanzibar, ili kuunda chama kipya, Chama cha Mapinduzi (CCM); ili kiwe ni chombo chenye uwezo na nguvu kubwa Zaidi ya kuongoza nchi yetu.Mfano wa tatu ni pale alipofanikiwa kuwaridhisha kwa kutumia nguvu ya hoja zake, wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TANU uliofanyika Tabora mwaka 1958, wakakubali sheria ya, “kura tatu” iliyokuwa imetungwa na Serikali ya Kikoloni wakati huo. Nguvu ya hoja yake ilikuwa ni kwamba kama mkutano huo ungeamua kukataa sharia hiyo, chama cha TANU kisingeruhusiwa kushiriki katika uchaguzi uliokuwa umepangwa kufanyika mwezi September mwaka huo; na matokeo yake yangekuwa ni kuchelesha kupatikana kwa Uhuru wa Tanganyika. Hali halisi iliyokuwepo ni kwamba wajumbe walio wengi katika mkutano huo, walikuwa wamejiandaa kuikataa sheria hiyo ya “kura tatu” Mwalimu Nyerere aliarifiwa mapema kabla ya mkutano kuhusu msimamo huo wa wajumbe, kwa hiyo yeye pia akaandaa mkakati wake mapema. Kwanza aliomba mkutano uchague mwenyekiti mwingine (wa muda) wa mkutano huo, ili yeye aweze kutoa hoja zake mkutanoni akiwa kama mjumbe wa kawaida, ili kuepuka kishawishi cha kutumia mamlaka ya “kiti” kulazimisha wajumbe kukubali mawazo yake.
                  Kutokana na uwezo wake huo wa kuridhisha watu kwa kutumia “nguvu ya hoja” ulivyo mkubwa, ingawa katika mkutano huo kazi hiyo ilikuwa ngumu sana, lakini bado  aliweza kuwaridhisha wajumbe, wakaikubali sheria hiyo. Uamuzi huo ulibadilisha kabisa historia ya Tanganyika , kwani ulisababisha Uhuru wa Tanganyika kupatikana katika muda mfupi sana wa miaka saba tu baada ya chama cha TANU kuundwa, mwaka 1954.
              Halikadhalika, ni uwezo wake wa kuridhisha watu kwa “nguvu ya hoja” zake, ndio uliofanikisha harakati zake  za kuunganisha maelfu kwa maelfu ya wananchi wa Tanganyika katika kudai Uhuru wa Tanganyika. Alifanikiwa kufanya hivyo kwa hotuba zake zilizoweza kuwafanya wananchi wabaini ubaya na aibu ya kutawaliwa na wakoloni; na kuwafanya wawe tayari kujitolea na kujituma  kushiriki katika harakati hizo. Ilibidi watu wajitole, kwa sababu TANU wakati huo haikuwa na vitendea kazi kama magari wala fedha za kufanyia kazi hiyo.

Maoni ya watu wengine kuhusu sifa za Mwalimu Nyerere
Sifa za Mwalimu Nyerere zimeelezwa kwa namna tofauti na watu wengi wengine waliomfahamu. Kwa mfano, katika kumkaribisha kuhutubia mkutano ulioandaliwa na “African American Institute” ya huko Marekani tarehe 10 Feburuari, 1960; mshehereshaji wa hafla hiyo alimtambulisha Mwalimu Nyerere kwa maneno yafuatayo:
“Mr. Nyerere has won the confidence of all groups in Tanganyika by his wisdom, modesty and humour”.
(Bwana Nyerere ameaminiwa na makundi yote ya huko Tanganyika kutokana na busara zake, unyenyekevu wake na ucheshi wake).

Naye mwandishi Peter Haussler, katika kitabu chake kiitwacho, “Leadership for Democratic Development in Tanzania,” aliandika kuwa:
“The leadership style of Nyerere is also referred to as “charismatic” and “visionary”. Charismatic leadership is the ability to influence followers based on supernatural gifts and attractive powers. Followers enjoy being with the charismatic leader because they fell inspired, correct and important”.
(Uongozi wa Mwalimu Nyerere umeelezwa mara nyingi kuwa ni wenye haiba kubwa, wa mtu mwenye kuona mbali. Kiongozi mwenye haiba ni yule mwenye uwezo wa ajabu wa kuwawishi na kuvutia watu, aina ya uwezo ambao si wa dunia hii. Wafuasi wake wanafurahia kuwa karibu naye kwa sababu anawatia moyo, wanajiona kuwa wako sahihi, na ni watu wenye maana).
Vilevile, katika kijitabu kinachoitwa, “Memories of Julius Nyerere”, kilichochapishwa mwaka 2009 kama sehemu ya maadhimisho ya miaka kumi ya kifo chake, ambacho kilichangiwa na waandishi kadhaa, mwandishi mmoja alimweleza kuwa:
“Nyerere was an iconic leder, a man of principle, intelligence, and integrity”. 
(Nyerere alikuwa ni kiongozi mwenye taswira ya pekee, mwenye kusimamia misingi na maadili mema, na mwenye akili nyingi).
Mwndishi mwingine alimweleza Mwalimu Nyerere kuwa:
“He was considered a political prophet by many, and a man of intelligence, humour and honesty’
(Wengi walimwona kuwa ni kama nabii wa kisiasa, na mtu mwenye maadili mema, mchangamfu mwenye ucheshi, na mkweli).

Mimi mwenyewe vilevile nilipewa nafasi ya kuchangia Makala katika kijitabu hicho ambapo nilisema hivi:
“Nyerere has been variously described as a humanist, politician, thinker, and statesman. Indeed, Nyerere was all of those things and much more. He was an ardent believer in peace, and a unque mobilizer of people. He was a devout catholic, but a strong believer in the separation of religion from politics. He was 
a modest man in his personal life, and hated pomposity in his official life”
(Nyerere ameelezwa na watu wengi mbalimbali kwamba alikuwa ni mpenda watu, mwenye kufikiri sana, na mwanasiasa mweledi. Ni kweli kabisa kwamba, Nyerere alikuwa na sifa zote hizo, pamoja na nyingine Zaidi. Kwani alikuwa ni muumini mkubwa katika suala la Amani, na hodari sana wa kuandaa watu. Alikuwa ni mfuasi mwaminifu sana wa dini Katoliki, lakini hakupenda kabisa kuchanganya dini na mambo ya siasa. Alikuwa ni mtu mwenye staha katika maisha yake binafsi, na alichukia sana ufahari katika maisha yake kama kiongozi).
Katika dondoo la kueleza sifa za Nyerere lililosomwa na Waziri Mkuu wa India, Bibi Indira Gandhi, katika sherehe za kumkabidhi tuzo ya, “Jawaharlal Nehru Award for International Understanding” tarehe 17 Januari, 1976, Mwalimu Nyerere alitajwa kuwa :
“A man of vision, a man of action, and a man of compassion”.
(Mtu mwenye kuona mbali, mtu wa vitendo, na mtu mwenye huruma).
Kabla ya hapo, katika sherehe hiyohiyo, Rais wa India alimweleza Mwalimu Nyerere kuwa:
“He is one of the foremost champions of human rights. He is a man of the people, gifted with great commonsense”
(Mwalimu Nyerere ni mmoja wa watu walioko mstari wa mbele katika kupigania haki za binadamu. Ni mtu wa watu, na amejaliwa kuwa na kiwango kikubwa mno cha maarifa na busara za kawaida).
Kwa ujumla, katika maisha yake yote, Mwalimu Nyerere alidhihirisha kwamba alikuwa na sifa zote hizo, kwani alitekeleza ipasavyo misingi yote ya maadili mema, siyo tu katika maisha yake binafsi, bali pia katika maisha yake ya uongozi. Na alifanya hivyo katika kipindi chote cha uhai wake, kama inavyobainishwa katika maelezo yanayofuatia hapa chini:

MAISHA BINAFSI YA MWALIMU NYERERE
Kuhusu maisha yake binafsi, Mwalimu Nyerere alikuwa na sifa zifuatazo:
  1. Alikuwa ni mtu mwadilifu sana, asiyekuwa na makuu, mtu mwenye staha, mtu aliyetosheka; na asuyekuwa n ahata chembe ya majivuno.
Kwa mfano, alipoanza kushika wadhifa wa Rais, hakupenda hata kidogo kujihusisha na zile mbwembwe ambazo kwa kawaida huambatana na wadhifa huo. Ifuatavyo ni mifano michache inayothibitisha tabia yake hiyo:
             Baadhi ya watu waliomfahamu alipokuwa mwanafunzi katika shule ya sekondari Tabora, wameeleza kwamba hata wakati huo akiwa bado mwanafunzi, tayari alikwisha kujenga tabia ya kuchukia marupurupu ya upendeleo (privileges) yaliyokuwa yakitolewa kwa wanfunzi wenye  nafasi za uongozi, yaani viranja. Hatimaye msimamo wake huo ulidhihirika wakati yeye mwenyewe alipochaguliwa kuwa kiranja, ambapo alitumia kipaji chake cha ushawishi, kupunguza marupurupu ya cheo hicho cha viranja wa wanafunzi katika shule hiyo.
            Mfano mwingine nilioushuhudia mimi mwenyewe, ni kwamba alipokwisha kuchaguliwa na kuapishwa kuwa Rais wa Tanganyika tarehe 9 Desemba, 1962, shughuli yake ya kwanza ilikuwa ni kulifungua na kulihutubia Bunge la Kwanza la Jamhuri ya Tanganyika siku ya kesho yake tarehe 10 Desemba, 1962. Mimi wakati huo nikiwa Katibu wa Bunge, ndiye nilikuwa mwandalizi wa ratiba ya shughuli hiyo kubwa.




Nilijaribu kuiga   ratiba ambayo hutumika katika Bunge la Uingereza (House of Commons) wakati Malkia wao anapokwenda kuhutubia Bunge hilo mwanzoni mwa kila mwaka wa shughuli zake. Katika sherehe hizo huwa anasindikizwa na Afisa mmoja wa kike ambaye cheo chake kinaitwa, “Lady-in-Waiting”. Kwa kuwa nilikuwa nimesomeshwa kazi za Ukatibu wa Bunge katika Bunge hilo la Uingereza, niliamini kuwa huo ndio utaratibu unaofaa kutumiwa pia katika Bunge jipya la Tanganyika. Kwa hiyo nikapanga kuweka ndani ya ukumbi wa Bunge sambamba na kiti cha Rais mwenyewe, kiti cha mke wa Rais Mama Maria Nyerere, na kiti cha msindikizaji wake wa kike, ambaye nilimwonyesha katika ratiba yangu ya shughuli hiyo kwa cheo hicho nilichokijua cha “Lady-in- Waiting”.

         Kumbe Rais Nyerere hakupendezwa na mbwembwe hizo. Aliziona kuwa ni za Kisultani, zinazofaa kwa Masultani tu. Kwa hiyo baada ya tukio hilo alituagiza tuachane kabisa na mbwembwe hizo, alizoziita ni za kijinga.
        Wakati huo, vilevile watu walikuwa wameanza kutumia maneno, “Mtukufu Rais” katika hotuba zilizomtaja yeye, au katika barua zilizokwenda kwake. Kuzuia hilo, aliandika waraka wa kuagiza kwamba asiitwe, “Mtukufu Rais” wakati wowote na mahali popote; iwe ni katika mazungumzo ya kawaida, ama katika hotuba, au hata katika maandishi yoyote. Akaelekeza kwamba, maneno rasimi katika mawasiliano ya aina hiyo yawe ni “Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Rais wa Tanganyika” na si vinginevyo. Aidha katika utaratibu wake wa kukataa mbwembwe, Rais Nyerere pia aliwaagiza polisi waache tabia yao ya kufunga kila barabara anayopita Rais, kwa muda usiojulikana, hadi hapo Rais atakapokuwa amepita. “Hii inanifanya niwe kero kubwa kwa watu wa Dar Es Salaam”, alisema.





  1. Alikuwa ni mtu asiyependa kujilimbikizia mali
Hii ni tabia yake nyingine ambayo inamtofautisha na viongozi wengine wengi duniani wa ngazi hiyo kubwa katika Mataifa yao.
           Kwa mfano, Mwalimu Nyerere hakuwahi kununua gari lake mwenyewe binafsi na kwa ajili hiyo, hakuwahi hata kujifunza kuendesha gari.
         Wakati alipokuwa mwalimu katika shule ya sekondari Pugu, sisi wanafunzi tulishuhudia siku moja akipanda nyuma ya gari la shule aina ya pick-up single cabin. Alikuwa anakwenda mjini Dar Es Salaam, bila shaka kwenye shughuli zake za kisiasa alizokuwa amezianza wakati huo. Katika kiti cha mbele walikuwa wamekaa walimu wenzake Mapadre wawili Wazungu wa Shirika la “Holy Ghost Fathers”. Sisi wanafunzi tulidhani alikuwa amefanyiwa dharau ya ubaguzi wa rangi na Mapadre hao wazungu.
          Baadaye katika mazungumzo naye nje ya darasa, mwanafunzi mwenzetu mmoja allimweleza Mwalimu Nyerere hisia zetu hizo, tulipomwona akipanda nyuma ya gari la shule “kama mzigo”. Majibu ya Mwalimu Nyerere yalikuwa kwamba Mapadre walikuwa wamemwambia akae pamoja nao katika kiti cha mbele. Lakini yeye alikataa kwa sababu hakuona haja ya kubanana kwenye kiti hicho, wakati nyuma ya gari palikuwa na nafasi kubwa ya kukaa. Ndiyo sababu aliamua kukaa nyuma ya gari. Kwa hakika, Mwalimu Nyerere hakuwa na makuu.
         Mfano mwingine wa tabia yake ni kwamba mnamo mwezi Januari mwaka 1976, Mwalimu Nyerere alitunukiwa tuzo maarufu ya “Jawahrlal Nehru Award for International Understanding”. Tuzo hiyo inaambatana na zawadi ya kiasi kikubwa cha dola za Kimarekani, kama dola laki moja. Yeye baada ya kuzipokea fedha hizo alizikabidhi zote kwa Chuo cha TANU cha Kivukoni ili zitumike kanunulia vitabu vya maktaba ya chuo hicho. Ni Dhahiri kwamba hakuwa na tabia ya kujilimbikizia mali.
         Ukiacha mifano hiyo, Mwalimu Nyerere mwenyewe aliwahi kutusimulia hadithi moja, kwamba katika safari zake za kwenda kudai uhuru kwenye Umoja wa Mataifa huko New York – Marekani, safari moja alikutana na rafiki yake ambaye alikuwa anaishi huko. Rafiki yake huyo akamwambia kuwa angependa kumununulia zawadi ya viatu lakini kwa kuwa alikuwa hajui saizi yake ya viatu, akamshauri waende wote dukani ili akamnunulie viatu vya saizi inayomfaa.
        Mwalimu Nyerere akakubali kupokea zawadi hiyo, wakaenda duka la viatu ambako alichagua jozi moja ya viatu vya rangi nyeusi. Rafiki yake huyo akamshawishi achague jozi ya pili, lakini Mwalimu Nyerere alikataa. Rafiki yake akamuuliza kwanini hataki jozi ya pili, Mwalimu akamjibu hivi; si kwa  sababu ninayo jozi moja tu ya miguu! (I have only one pair of feet!) kwa hakika hakutaka kujilimbikizia mali hata kama mali, hiyo ni viatu tu.

  1. Alikuwa ni mtu mwenye kumtegemea sana Mungu
Jambo hilo lilikuja kudhihirika miaka kumi baada ya kifo chake, ambapo kanisa Katoliki Jimbo la Musoma, lilipoanzisha mchakato wa kumfanya hayati Mwalimu Nyerere kuwa ni “Mtakatifu wa Mungu”. Hatua ya kwanza muhimu katika safari ya kuelekea kwenye daraja la Mtakatifu wa Mungu ni kutangazwa kuwa “mtumishi wa Mungu”, ngazi ambayo Mwalimu Nyerere tayari amekwishaifikia. Baada ya kuanza kwa mchakato huo. Kanisa Katoliki nchini Uganda, lilishirikiana na Rais Museveni wan chi hiyo; limeshiriki kwa nguvu katika kuendeleza mchakato huo. Kwani kuanzia mwaka 2007, kanisa  hilo la Uganda lilitenga tarehe 1 Juni ya kila mwaka kuwa ni siku ya kuombea mafanikio ya mchakato huo. Maadhimisho hayo hufanyika mahali panapoitwa “Namugongo” huko Kampala Uganda. Katika maadhimisho ya mwaka 2011, Rais Yoweri Museveni wa Uganda alitangaza kuwa;
“We shall continue comimg back here every June 1 to pray for the beatification of our beloved father, which is the next stage. Then we will always pray for him to be canonized.”
(Tutaendelea kuja hapa Namugongo kila tarehe 1 ya mwezi Juni, kuombea mafanikio ya mchakato huu wa kumfikisha baba yetu mpendwa kwenye Daraja la “Mwenye Heri” ambayo ndiyo hatua inayo fuatia baada ya hapo tutaendelea kumwombea afikishwe kwenye daraja la juu zaidi la Utakatifu).
Kwa hakika Mwalimu Nyerere alikuwa ni mcha Mungu sana, kutokana na tabia yake ya kuhudhuria Ibada ya Misa Takatifu kila siku asubuhi, katika kanisa la Mt. Petro Oysterbay, ambalo lilikuwa la karibu Zaidi na nyumbani kwake Msasani. Lakini vilevile alikuwa na tabia nzuri ya kuomba uongozi na msaada wa Mwenyezi Mungu wa kumuwezesha kufikia uamuzi wa busara katika masuala yaliyokuwa nyeti na magumu kwake.
          Mfano mmoja ambao unadhihirisha tabia yake hiyo, ni jinsi alivyofikia uamuzi mgumu wa kuruhusu majeshi ya Tanzania yavuke mpaka na kwenda Kampala kumwadhibu vikali aliyekuwa Mtawala wa Uganda wakati huo, Iddi Amin Dada, aliyekuwa maefanya uvamizi wan chi yetu katika mkoa wa Kagera, Nitasimulia habari hii zaidi hapo baadaye.





  1. Hata alipokuwa Rais aliishi maisha ya mtu wa kawaida.
Ingawa alikuwa na nafasi ya juu kabisa na yenye heshima kubwa katika jamii, ya kuwa ni Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania; lakini bado Mwalimu Nyerere alichagua kuishi maisha ya mwananchi wa kawaida. Kwani aliishi maisha yake yote kama wanavyoishi wananchi wa kawaida, wasiokuwa na uwezo mkubwa wa kifedha. Katika hilo, kaulimbiu yake ilikuwa ni “Kiongozi wa watu lazima afanane na watu anaowaongoza”.
           Kwa mfano nyumba yake aliyokuwa akiishi pale kijijini kwake Butiama, ni iliile aliyoijenga akiwa bado kijana, katika maandalizi ya kufunga ndoa na Mama Maria Nyerere. Lakini hata baada ya kuwa Rais wan chi, bado aliendelea kuishi katika nyumba hiyo ndogo ya chumba kimoja tu cha kulala. Kwa sababu hiyo, alipotangaza katika Mkutano Mkuu wa Tanu wa kumteua kuwa mgombea Urais mwezi September 1975, kwamba angestaafu kazi ya urais ifikapo mwaka 1980; chama cha Tanu kilipitisha azimio la kumpatia zawadi ya kumjengea nyumba bora Zaidi katika kijiji chake cha Butiama, ambayo ataitumia kama makazi yake baada ya kustaafu.
          Nyumba hiyo aliyohaidiwa ilianza kujengwa mwaka 1977, mara baada ya kuzaliwa kwa CCM, ujenzi ambao ulikamilika mwaka 1980. Mimi nikiwa Katibu Mtendaji Mkuu wa CCM wakati huo, ndiye niliyepewa heshima ya kuikabidhi nyumba hiyo mpya kwake na familia yake, katika sherehe fupi iliyofanyika hapo Butiama mwezi Desemba 1980.
        Aidha, kwa upande wa makazi yake ya Dar Es Salaam, Mwalimu Nyerere alijijengea mwenyewe nyumba hiyo alipokuwa tayari amekwisha kushika wadhifa wa Rais wan chi yetu, kwa kutumia mkopo wa Benki. Ujenzi wake ulipokamilika tu, alihama kutoka Ikulu na kwenda kuishi kwenye nyumba yake hiyo ya Msasani, ambako aliendelea kuishi hadi mwisho wa maisha yake hapa duniani.
          Mfano mwingine tena wa uadilifu wake, ni wakati alipopelekewa pendekezo la kujengewa barabara ya lami kutoka kijijini kwake Butiama hadi sehemu inayoitwa Makutano, ili kuiunganisha na barabara ya lami inayotoka Musoma kwenda Mwanza, kwa lengo la kufanya makazi ya Rais kule Butiama yaweze kufikika kwa barabara ya lami. Lakini Mwalimu Nyerere alikataa kuidhinisha pendekezo hilo, kwa maelezo kwamba hakutaka fedha za umma zitumike katika kumpendelea yeye kutokana na Urais wake, wakati mahitaji ya wananchi wengine yalikuwa ni makubwa Zaidi.

  1. Alikuwa ni msomi ambaye ni mfano wa kuigwa
Mwalimu Nyerere alikuwa na tabia nzuri sana ya kusoma vitabu. Kwa ajili hiyo alikuwa na maktaba yake binafsi yenye vitabu vingi sana nyumbani kwake Msasani, na vilevile nyumbani kwake Butiama.
          Ni kutokana na kutambua tabia yake hiyo ya kupenda kusoma vitabu, ndiyo sababu alipostaafu wadhifa wa Urais wa nchi mwaka 1985, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania liliamua kumzawadia seti nzima ya vitabu 33, vinavyoitwa Encyclopaedia Britanica. Watu wengi wanakumbuka jinsi makundi mbalimbali ya wananchi wa Tanzania, pamoja na baadhi ya watu binafsi; walivyojipanga kumpatia Mwalimu Nyerere zawadi nyingi za aina mbalimbali wakati alipostaafu Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wengine walitoa zawadi ya ng’ombe, wengine walitoa matrekta ya kulimia na kadhalika. Zawadi ya Chama cha Mapinduzi ilikuwa ni kumjengea nyumba ya kuishi Kijijini kwake Butiama. Halikadhalika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), vilevile ilimjengea nyumba ya kuishi Butiama. Lakini Bunge liliamua kumuzawadia vitabu.
       Pamoja na kupenda kusoma vitabu, Mwalimu Nyerere pia alikuwa ni mwandishi hodari wa vitabu, pamoja na Makala fasaha za aina mbalimbali, zikielezea mambo tofautitofauti. Baadhi ya hizo aliziandika kwa lugha ya Kiswahili, na nyingine akiziandika kwa lugha ya Kingereza, hususani zile zilizolenga wasomaji wake wa Kimataifa. Miongoni mwa hizo ni, “Principles and development”; “Stability and Change in Africa”; “The Honour of Africa” na “The South-South Option”
Lakini juhudi zake za kisomi zinazozoshangaza zaidi, ni pale alipofanya kazi ya kutafsiri vitabu maarufu vilivyoandikwa kwa kingereza, na kuviweka katika Lugha ya Kiswahili. Vitabu hivyo maarufu ni pamoja na sehemu ya Agano jipya la Biblia Takatifu, ambayo ni injili zote nne, kama zilivyoandikwa na watakatifu MATHAYO; MARKO; LUKA; YOHANA. Tafsiri yake inaitwa TENZI ZA BIBLIA, vitabu hivyo vilichapishwa na Peramiho Mission Press, Songea). Vitabu vingine alivyovitafsiri kwa Kiswahili ni vile vilivyoandikwa na mwandishi maarufu wa fasihi za kingereza Wiliam Shakespeare, ambavyo ni JILIUS CAESAR na THE MERCHANT OF VENICE
Kuhusiana na juhudi zake hizo, jambo kubwa zaidi na la kushgangaza kabisa, ni je, alipata wapi muida wa lutosha kufanya kazi hiyo? Ikizingatiwa kwamba Toleo la kwanza la Tafsiri ya Julius Caeser ( kwa Kiswahili: Julias Kaizari) lililochapishwa na shirika la Oxford University Press, lilitoka mwaka 1967;  miaka ambayo ni dhahiri mwalimu Nyerere alikuwa katika harakati nzito za kuijenga nchi yetu changa, mara baada ya kupatikana na uhuru mwishoni mwa mwaka 1961; pamoja na harakati nyingine za ukombozi wan chi zingine za Bara la Afrika kutoka  katika kutawaliwa na wakoloni; inashangaza kuona kwamba mwalimu Nyerere, aliyekuwa mtumishi wa umma nambari moja, aliweza kupata muda wa kufanya hivyo, inakuwaje wengine, wenye majukumu madogo zaidi kuliko aliyokuwa nayo yeye, wanashindwa?
Mchango  wa mwalimu Nyerere katika kustawisha Kiswahili
Juhudi za mwalimu Nyerere za kutafsiri vitabu hivyo na kuviweka katika lugha ya Kiswahili, zilikuwa na sababu nyingine kubwa  ambayo yafaa pia kuifahamu. Sababu yake ilikuwa ni kuonesha utajiri wa lugha ya Kiswahili ulivyo mkubwa, kiasi kwamba kinayo maneno ya kutosha, sawa na fasihi za Lugha ya kingereza, kilichokuwa kinatumika mashuleni kama lugha ya kufundishia.
Lakini siyo hilo tu. Jitihada za Mwalimu Nyerere za  kutukuza Kiswahili zilianza mapema zaidi, mara tu baada ya kupatikana uhuru wa nchi yetu; ambapo Mwalimu Nyerere, (akiwa ndiye kiongozi Mkuu wa nchi), alitangaza Kiswahili kuwa ndiyo lugha rasmi ya taifa letu. Maana ya tanzazo hilo ilikuwa ni kwamba shughuli zote za serikali (ambazo ilikuwa inawezekana kuziendesha kwa kiswahili), ilibidi sasa ziendeshwe kwa lugha hiyo ya Taifa. Na papo hapo iliamliwa pia kwamba shughuli za mijadala ya Bunge  zianze mara moja kuendeshwa kwa lugha ya Kiswahili. Na ndipo neno ‘Bunge’ lilipobuniwa, kutokana na neno la Kiganda “BULANGE”; lenye maana ya ‘Bunge la Buganda’ (inayotawaliwa na Mfalume Kabaka ndani ya Jamuhuri ya Uganda)
Kwa upande wa Elimu yake ya darasani, mbali na shahada yake ya M.A. aliyotunukiwa baada ya kufaulu masomo katika chuo Kikuu cha Edinburgh, Uingereza;  vile vile alitunukiwa shahada nyingine nyingi za heshima (honorary Degrees) na vyuo vikuu mbalimbali duaniani; ambavyo ni pamoja na Edinburgh (uingereza); Duquesne (marekani); Cairo (Misri); Nsukka (Nigeria); Ibadan (Nigeria); Harare (Zimbabwe); Monrovia (Liberia); Toronto (Canada); Howard (Marekani); Jawahral Nehru (India); Havana (Cuba); Lesotho  (Lesotho); The Philipines (Ufilipino); na Fort Hare (Afrika Kusini).
MAISHA YA MWALIMU NYERERE KAMA KIONGOZI
Katika maisha yake kama kiongozi wa nchi, Mwalimu alitawaliwa kwa kiwango kikubwa sana na Imani thibiti aliyokuwa nayo; kwamba “binadamu wote ni sawa”, na kwamba “kila mtu anastahili kuheshimiwa na kuthaminiwa utu wake”.
Mifano michache iliyotolewa hapo juu inasaidia kuthibitisha kwamba imani yake hiyo ndiyo ilikuwa msingi mkubwa wa uamuzi wake mwingi aliokuwa akiufanya katika kipindi cha uongozi wake. Vielelezo vya utekelezaji wa imani yake hiyo, ni kama ifuatavyo:-
  1. Alichukizwa sana na dhuluma, uonevu, na upendeleo
Kuhusu juhudi zake za kupambana na dhuluma na uonevu katika jamii, ipo mifano kadhaa ya vitendo vyake vinavyodhihirisha mapambano hayo. Kwanza, mapema mwaka 1963, muda mfupi tu baada ya kushika madaraka ya Rais wa Tanganyika, Mwalimu Nyerere alitoa amri ya kufuta Kodi iliyokuwa inaitwa ‘kodi ya kichwa’. Kodi hii ilikuwa ikitozwa kwa  kila mtu mzima, bila kujali uwezo wake wa kulipa. Alifuta kodi hiyo kutokana na kitendo kilichomuudhi sana cha kukamatwa kwa baadhi ya wananchi waliokuwa wameshindwa kuilipa. Walioswekwa ndani katika mahabusu moja katika kijiji cha ilemela, Karibu na mji wa Mwanza
Kutokana na msongamano ulivyokuwa mkubwa katika mahabusu hiyo, baadhi ya watu hao walifariki dunia. Habari hizo zilipomfikia Rais Nyerere, aliamuru kufutwa kwa kodi hiyo mara moja, kwani aliona kuwa ilikuwa inasababisha dhuluma na uonevu kwa wananchi walio wengi
Baadaye tutaona mifano mingine ya vitendo vyake vilivyotokana na tabia yake hiyo ya kuchukia dhuluma, unyanyasaji, ubaguzi, Uonevu,  na hata upendeleo usiofaa.
  1. Alikuwa ni jasiri wa kufanya uamuzi mgumu na nyeti
Ujasiri wake wa kufanya uamuzi mzito na mgumu, ulitokana na msimamo wake imara na usiotetereka wa kutetea misingi aliyokuwa  anaiamini kwa dhati. Msimamo huo ulidhihirika tangu mwanzoni kabisa mwa kipindi cha uongozi wake, hata kabla ya kupata uhuru, Baadhi ya mifano ya vitendo vyake katika kipindi hicho ni hii ifuatayo:
Kama sehemu ya mapambano aliyokuwa akiyaongoza dhidi ya ubaguzi wa rangi uliokuwa ukifanywa na Serikali za makaburu wa Afrika Kusini, pamoja na udhalimu wa serikali ya Ureno iliyokuwa inatawala Msumbiji, mara tu alipopata madaraka ya kumwezesha kufanya hivyo, alifanya uamuzi wa kijasiri sana  unaoelezwa katika kifungu hiki. Ulikuwa uamuzi wa kijasiri kwa sababu, kwa kiasi Fulani, aliathiri uchumi wa Tanganyika. Bila shaka, Rais Nyerere alitambua kuwapo kwa athari hizo, lakini alitetea uamuzi wake huo kwa maelezo kwamba hizo zilikuwa ni gharama za kusimama kwenye misingi (the cost of principle); ambazo ilikuwa ni lazima kuzibeba kwa ajiri ya kutetea misingi hiyo:

  1. Alisusia bidhaa za Afrika Kusini
kuhusu Afrika Kusini, Mwalimu Nyerere alifanya mambo yafuatayo:
kwanza, alipiga marufuku uingizaji nchini Tanganyika wa bidhaa zozote kutoka Afrika Kusini.
Pili, alitangazia ulimwengu kwamba endapo Afrika kusini itaendelea kuwa mwanachama wa Jumuiya ya Madola, basi Tanganyika itakapopata uhuru wake haitajiunga na Jumuiya hiyo. Alieleza kuwa yeye, kama kiongozi wa Tanganyika huru, asingeweza kukaa meza moja na kiongozi wa serikali inayoendesha sera za ubaguzi kama hiyo ya Afika Kusini, katika vikao vya Jumuiya hiyo ya Madola.
Alifanya hivyo akijua athari zake kwa uchumi wa Tanganyika, ambao zingetokana na kutojiunga na Jumuiya ya Madola, kwani nchi hii ingekosa nisaada kutoka katika mataifa kama Uingereza na Canada, pamoja na kukosa nafuu za kibiashara (trade preferences) zilizokuwa zikitolewa kwa wanachama wa jumuiya hiyo. Lakini bado akawa na ujasiri wa kutoa kauli hiyo nzito.
Ilitokea bahati njema kwamba, kauli yake hiyo ilizaa matunda mazuri. Kwani tangazo lake hilo liligeuka kuwa shinikizo la kutosha kusababisha Serikali ya Afrika Kusini ijiondoe yenyewe katika uanachama wa Jumuiya hiyo. Baadaye Mwalimu Nyerere alitusimulia kuwa yeye mwenyewe hakuwa na matumaini kwamba kauli yake hiyo ingesikilizwa na wahusika, na kwamba yeye alikuwa hajapata habari ya matokeo hayo mpaka waziri wake Amir Jamal alipokwenda nyumbani kwake kumpasha habari hizo alizokuwa amezisikia kwenye matangazo ya BBC, kuwa serikali ya Afrika Kusini imejiondoa yenyewe katika Jumuiya ya Madola. Alituambia jinsi alivyopata mshangao wa furaha, kwani hakuwa ametegemea kupata matokeo mazuri na kwa haraka kiasi hicho.
  1. Alivunja uhusiano na Ureno
Mwalimu nyerere alivunja uhusiano wa kibihashara na Ureno, kwa sababu ya vitendo vya udhalimu alivyokuwa vikifanywa na nchi hiyo katika koloni lake la Msumbiji. Alifanya hivyo huku akijua kwamba uhusiano huo ungeendelea kuwepo, pengine angeweza kusaidia katika kuweka msimao wa pamoja wa kibihashara katika Nyanja za kimataifa, hususan bei za korosho na Mkonge, mazao ambayo yanalimwa katika Nchi zote mbili. Lakini kwa msingi wa kupambna ma udhalimu, bado alikataa uhusiano huo usiwepo.

  1. Alijitolea  kuunga mkono harakati za ukombozi wan chi za kusini mwa Afrika
Msimamo wake wa kusaidia kwa hali na mali juhudi za ukombozi wa nchi za kusini mwa afrika, ziliiweka nchi yetu katika hatari kubwa ya kushambuliwa kijeshi na nchi ambazo wapigania uhuru wake walihifadhiwa na kulindwa katika kambi kadhaa zilizokuwepo hapa nchini. Hatari hiyo ilizidi kuwa kubwa baada ya kukubali nchi yetu kuwa mwenyeji wa kamati ya ukombozi ya umoja wa Afrika (OAU Liberation Committee), ambayo ofisi zake ziliwekwa mjini Dar es salaam. Huo ulikuwa ni mchango mahususi wa Mwalimu Nyerere katika jitihada zake za kupinga dhuluma ya nchi hizo kutawaliwa na wakoloni. Lakini ulikuwa ni uamuzi mgumu sana kuufanya katika mazingira ya wakati huo yalivyokuwa.

  1. Alikataa misaada ya Ujerumani
Mara baada ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar, kulitokea mgogoro wa kidplomasia ambao ulimsababisha Mwalimu Nyerere kufanya uamuzi mwingine mgumu, wa kuikataa misaada yote ya Ujerumani iliyokuwa imepanga kuitoa kwa nchi yetu. Wakati huo, ujerumani ilikuwa ni nchi mbili tofauti: Ujerumani ya mashariki na Ujerumani ya Magharibi. Ujerumani ya magharibi peke yake ndiyo ilikuwa na uhusiano wa kibalozi na Tanganyika kabla ya Muungano, na ilikuwa ikitoa misaada mingi kwetu.
Mara baada ya Mapinduzi ya Zanzibar, Ujerumani ya Mashariki ilifungua uhusiano wa kibalozi na Zanzibar. Tukio hilo lilisababisha Ujerumani ya Magharibi kudai kwa nguvu,  kwamba Tanzania isiruhusu kuwapo kwa ubalozi wa Ujerumani ya Mashariki hapa nchini, kwa maana ya Zanzibar. Mashinikizo hayo yalitokana na msimamo wao wakati huo, uliojikita kwenye dhana iliyojulikana kwa jina la ‘Halshtein Doctrine’, dhana ambayo haikuruhusu kuwapo kwa uwakilishi wan chi zote mbili za Ujerumani katika nchi moja yoyote ya kigeni. Sababu yake ilikuwa kwamba Ujerumani ya Magharibi ilikuwa haitambui kabisa kuwepo kwa nchi inayoitwa Ujerumani ya Mashariki.
Katika kutafuta ufumbuzi  wa mgogoro huo, Rais Nyerere, kwa kutumia utaratibu wake wa kushawishi kwa kutumia “nguvu ya huja”, alishauri Ujerumani ya magharibi ikubali utumike utaratibu ambao tayari ulikuwa umekubaliwa utumike katika nchi ya Misri, ambapo Ujerumani ya Magharibi ilikuwa Ubalozi kamili, na ujerumani Mashariki pia alikubaliwa kuwa na uwakilishi katika ngazi ndogo zaidi ya ‘Consulate –General’.
Lakini Ujerumani ya Magharibi haikuuafiki ushauri huo, na wala haikuishia hapo; bali ilichukua hatua ya kuvunja mkataba wa miaka mitano uliokuwepo wa nchi hiyo kutoa msaada wa mafunzo ya kijeshi kwa wanajeshi wetu wa anga. Vilevile walitoa pia tishio kwamba hata misaada yao mingine vilevile itaondolewa kama Serikali ya Tanzania haitabadili msimamo wake juu ya suala hilo. Rais Nyerere hakuwa ni mtu wa kuyumbishwa kwa vitisho kama hivyo. Kwa hiyo, akaamuru Serikali ya Ujerumani Magharibi iondoe mara moja misaada yake mingine yote.
Kwa hakika, alikuwa ni uamuzi mgumu, kwa sababu uliathiri nchi yetu kiuchumi. Kwa mfano, ulifuta kabisa uwezekano wa kupata msaada wa Ujerumani katika mpango wa kuendeleza Bonde la mto Kilombero, ambao tayari Serikali ya Ujerumani ilikwisha kuukubali pamoja na kusimamisha ujenzi wa jingo la Nkurumah Hall katika chuo kikuu cha Dar es Salaam
  1. Alivunja uhusiano wa kidiplomasia na Uingereza
Mnamo mwaka 1965, koloni la Uingereza lililokuwa likiitwa ‘southern Rhodesia’, lilijitangazia uhuru wake, bila idhini ya mwenye koloni lake hilo, yaani Serikali ya Uingereza. Kufuatia tukio hilo, Mawaziri wa nchi zote ambazo ni wanachama wa OAU, walifanya mkutano wa dharura mjini Addis Ababa,  kwa madhumuni ya kuzingatia tukio hilo, na kukubaliana juu ya hatua inayofaa kuchukuliwa na nchi za Afrika katika hali hiyo.
Tarehe 2 desemba, 1965, mkutano huo ulipitisha azimio la kuipatia Serikali ya Uingereza muda maalumu wa kuchukua hatua za kuzima uasi huo wa koloni lake hilo la ‘Southern Rhodesia’. Azimio hilo lilisema wazi kwamba endapo hadi kufikia tarehe 15 ya mwezi huo, serikali ya Uingereza haitakuwa imechukua hatua zozote za dhati kufanya hivyo basi nchi zote za umoja wa Afrika zitavunja uhusiano wa kidplomasia na Uingereza siku hiyo.
Serikali ya Uingereza haikuchukua hatua zozote zile. Kwa hiyo, bila kusita wala kuchelewa, ilipofika tarehe hiyo 15 Desemba, 1965, Rais Nyerere alitangaza kuvunjwa kwa uhusiano wa Kidiplomasia baina ya Tanzania na Uingereza, katika kutekeleza uamuzi huo OAU.
Vilevile, huo ulikuwa ni uamuzi mgumu, kwa sababu uliathiri uchumi wetu. Kwa mfano, kulikuwa na makubaliano ambayo tayari yalikwisha kufikiwa, ingawa mkataba wake ulikuwa bado haujasainiwa, ya kupata mkopo usiokuwa na riba kutoka Serikali ya Uingereza, wa paundi za kiingereza milioni 7.5. Fedha ambazo zingetumika kutekeleza baadhi ya miradi iliyokuwa imewekwa katika mpango wa maendeleo wa miaka mitano, uliokuwa unaanza kutekelezwa mwaka huo. Kutokana na tukio hilo, fedha hizo zilisitishwa  kutolewa (frozen) Ni vizuri kueleza hapa pia kwamba ulikuwa ni uamuzi mgumu kutokana na sababu nyingine, kwani ni nchi mbili tu jasiri za Tanzania na Ghana ndizo peke yake zilizochukua hatua ya kutekeleza uamuzi huo wa OAU. Nchi nyingine zote zilizobaki za Afrika hazikufanya hivyo, pamoja na kwamba zilikuwa zimeshiriki katika kupitisha Azimio hilo la Addis Ababa.
Inawezekana kuwa Mwalimu Nyerere alikuwa amehisi kuwa usaliti huo ungetokea kwani jana yake tarehe 14 desemba, 1965, alikwenda kulihutubia Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, tena alifanya hivyo kwa lugha ya Kiingereza badala ya Kiswahili, kuashirikisha kwamba alikusudia nchi hizo nyingine ziweze kumsikia moja kwa moja bila kusubiri tafsiri.
Hotuba hiyo ya mwalimu Nyerere baadaye ilichapishwa katika kijitabu maalumu kilichopewa jina la, ‘The Honour of Africa’, (Heshima ya Afrika) ambacho kinaeleza umuhimu wa Afrika kuheshimu uamuzi wake mwenyewe. Miongoni mwa mambo mengi ya msingi aliyoyasema katika hotuba yake hiyo, ni pamoja na kuuliza maswali ya msingi kabisa yafuatayo:
“Can Africa fail to implement its own resolution? Do Africa states meet in solemn conclave merely to make a noise? Or do they mean what they say? The purpose of that resolution was to show that, Africa requires action to be taken against smith. If that action is not taken, do we just shrug our shoulders and do nothing about it? Can we – the African states – honourably do nothing to implement our own resolution?”
(Hivi kweli Afrika inaweza kushindwa kutekeleza uamuzi wake yenyewe? Nchi za Afrika zinaweza kweli kukaa katika kikao rasmi, kwa madhumuni ya kupiga kelele tu? Siyo kwamba yale watakayoyasema yana maana? Madhumuni ya azimio hilo yalikuwa ni kuonesha kwamba Afrika inadai hatua zichukuliwe dhidi ya Smith (Waziri Mkuu wa Rhodesia ya Kusini aliyejitangazia uhuru). Kama hatua hizo hazitachukuliwa, je, tunakunja mikono tu na kusema kwamba hatuna la kufanya? Hivi kweli nchi za Afrika zitakuwa zimelinda heshima yake kama hazitachukuwa hatua za kutekeleza azimio letu wenyewe?)
Mifano yote hiyo inadhihirisha msimamo wake ulivyokuwa imara sana katika kusimamia na kutetea kwa gharama yoyote, misingi ambayo aliiamini kwa dhati.
UAMUZI MWINGINE MGUMU WA MWALIMU NYERERE
  1. Uamuzi wa kuchelewesha Uhuru wa Tanganyika 
Katika kumsaidia msomaji wa kitabu hiki aweze kumwelewa vizuri zaidi Mwalimu Nyerere, pamoja na sababu halisi za baadhi ya Uamuzi mwingine alikuwa akiufanya, tunaongeza mifano mingine ifuatayo.
Kwanza, ni uamuzi wake alioutangaza kwamba yuko tayari kuchelewesha uhuru wa Tanganyika kusubiri uhuru wa Kenya na Uganda, ili kuziwezesha nchi hizo tatu kuunda Shirikisho la Afrika Mashariki (East Africa Federation) baada ya zote kuwa zimepata uhuru. Ni wazi kwamba baadhi ya viongozi wenzake katika TANU, hawakupendezwa na uamuzi wake huo, na wangeweza kumletea matatizo makubwa kama nguvu yake ya kukubalika katika jamii isingekuwa ni kubwa kama ilivyokuwa.
  1. Uamuzi wa kuitambua Biafra
Kutokana na imani yake kubwa kuhusu usawa wa binadamu, Mwalimu Nyerere alichukizwa sana kila alipoona binadamu Fulani wanaonewa au wanadhulumiwa na watawala wao.
            Ndiyo sababu alichukia sana utawala wa makaburu wa Afrika Kusini, kwa jinsi ulivyokuwa ukiwadhulumu na kuwanyanyasa watu weusi wa nchi hiyo. Ni sababu hiyo hiyo ya kuchukia dhuluma, ndiyo pia iliyomfanya atangaze kuitambua Biafra kama nchi inayopigania haki yake ya kujitawala wenyewe. Uamuzi huo ulikuwa ni mgumu kwa sababu Biafra ilikuwa ni sehemu ya Jamuhuri ya Shirikisho la Nigeria; pamoja na Umoja wa nchi huru za Afrika ulikuwa umepisha Azimio la kutambua mipaka ya nchi za Afrika iliyoachwa na wakoloni. Kwa hiyo, Biafra kupigania kujitenga kutoka shirikisho la Nigeria ilikuwa ni kitendo cha kukiuka azimio hilo la OAU.
Lakini pamoja na hayo, baada ya kuona jinsi watu wa sehemu hiyo ya Biafra walivyokuwa wanaonewa na kudhulumiwa na utawala wa Shirikisho la Nchi hiyo, hali ambayo ilifanya waamue kuanzisha mapigano ya kutaka wajiondoe kwenye shirikisho hilo. Mwalimu Nyerere aliamua kuunga mkono juhudi zao hizo, ili waondokane na dhuluma zilizokuwa zinawakabili kutoka kwa watawala wa Shirikisho la Nigeria.
Kwake yeye Mwalimu Nyerere, dhambi ya ubaguzi au dhuluma kwa watu kama ile iliyokuwa ikifanywa na makaburu wa Afrika kusini, inabaki kuwa ni dhambi ileile hata inapofanywa na watawala Nigeria, ambao ni wazawa. Ni lazima ilaaniwe
Mimi nilibahatika  kuwa miongoni mwa wageni waliokuwepo Ikulu kuhudhuria mkutano wake na waandishi wa habari wakati wa kuwatangazia uamuzi  wake huo, na niliweza kushuhudia hisia zake zilivyokuwa kali dhidi ya uonevu wa serikali ya shirikisho la Nigeria kwa wananchi wa Biafra, wakati alipokuwa akitoa maelezo yake. Hata hivyo, hatimaye Biafra ilishindwa katika vita vyake hivyo vya kujitenga. Kwa hiyo, iliendelea kuwa ni sehemu ya Shirikisho la Nigeria. Lakini kwa kitendo chake hicho, yeye alikwisha kuonesha msimamo wake wa kupinga dhuluma na maonevu yanaofanywa na Serikali yoyote dhidi ya raia wake.

MWISHO WA MAISHA YAKE.

Ugonjwa na kifo cha Mwalimu Nyerere
Kabla ya kifo chake, mimi, wakati huo nikiwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ndiye nilipewa jukumu la kumpelekea Mwalimu Nyerere nyumbani kwake Butiama, vile vitabu vya zawadi iliyotolewa kwake na Bunge, name nilifanya hivyo kwa heshima kubwa na taadhima.
        Zawadi hizo zilichelewa kupelekwa, kwa sababu vitabu hivyo vya Encyclopaedia Britanica, havikuweza kupatikana madukani vikiwa tayari vimekwisha kuchapishwa. Kwa hiyo, ilibidi vichapishwe upya huko Uingereza, na kusafirishwa kuletwa hapa nchini. Mchakato huo haukukamilika mapema. Hatimaye vilipowasili, ilikuwa ni wakati wa Mkutano wa Bunge bajeti ya mwaka 1999/2000; ndipo tukapanga utaratibu wa kuvipeleka Butiama baada ya kumalizika kwa Mkutano huo wa Bajeti.
          Ni bahati mbaya sana kwamba Mwalimu Nyerere hakupata nafasi ya kuvisoma na kuvitumia vitabu hivyo. Hii ni kwa sababu siku nilipofika Butiama kumkabidhi zawadi yake hiyo, nilimkuta akiwa tayari ni mgonjwa, amelala kitandani. Alikuwa ameanza kuumwa yale maradhi ambayo baadaye, mwezi huohuo, ilibidi apelekwe kutibiwa katika hospitali ya St. Thomas mjini London. Pamoja na jitihada kubwa za madaktari wa huko, bado hakuweza kupona. Mwenyezi Mungu alimwondoa duniani alfajiri ya tarehe 14 Oktoba, 1999.

Nilipata bahati ya kumwona huko London kabla hajafariki.
Mimi nilipata fursa ya kwenda kumjulia hali Mwalimu Nyerere wakati alipokuwa mgonjwa huko London. Ilikuwa  ni tarehe 25 Septemba, 1999, nilipokuwa njiani nikirudi kutoka nchi ya Trinidad and Tobago iliyopo katika visiwa vya Carribean; ambako nilikuwa nimekwenda kuhudhuria mkutano wa kila mwaka wa Wabunge wa Jumuiya ya Madola (Commonwealth Parliamentary Association), nikiwa Spika wa Bunge la Tanzania. Katika mkutano huo, mimi nilipata bahati ya kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa kamati ya utendaji (Executive Committee) ya chama hicho cha wabunge wa Jumuiya ya Madola; baada ya kuwashinda wagombea wenzangu wawili mmoja kutoka Canada na mwingine kutoka Cyprus.
          Kwa mujibu wa katiba yake, mwenyekiti wa Kamati hiyo ndiye kiongozi Mkuu wa Chama hicho. Kwa hiyo, nilitaka kumpelekea Mwalimu nyerere habari njema ya ushindi wangu huo, kwani ratiba ya ndege ilikuwa inanipitisha London ili kuunganisha na ndege zinazokuja Dar ES Salaam. Nilipangiwa na ubalozi wetu wa London utaratibu wa kumwona mahali alipokuwa amelazwa, na nikapata nafasi ya kuongea naye vizuri kwa muda usiopungua saa moja na nusu hivi, kuanzia saa sita mchana. Kutoka hapo nilikwenda moja kwa moja uwanja wa ndege wa Gatwick, kupanda ndege ya kurejea Dar Es Salaam.

Nilivyopokea taarifa ya kifo chake.
Kesho yake asubuhi, nilikwenda kwa Waziri Mkuu, Fredrick Sumaye, kwa lengo la kumpelekea habari njema za kuchaguliwa kwangu kuongoza chama cha Wabunge wa Jumuiya ya Madola; pamoja na kumueleza nilivyopitia London kumjulia hali Mwalimu Nyerere, kwamba nilivyomwona na kuongea naye, alikuwa anaendelea vizuri na matibabu yake. Vilevile nilimjulisha Waziri Mkuu Mwalimu mwenyewe alivyokuwa ameniambia, kwamba alikuwa tayari amemwagiza Balozi wetu aliyepo London, amwandalie safari ya kurejea nyumbani wiki iliyokuwa inafuata; ili aweze kuja kukamilisha jukumu lake la kusuluhisha mgogoro wa Burundi. Lakini kumbe Mungu alikuwa na mpango tofauti kwake kwani baadaye siku hiyo hiyo, Balozi akaleta taarifa Serikalini kwamba hali ya Mwalimu Nyerere ilikuwa imebadilika ghafla jana yake jioni, na kwamba alikuwa amekata kauli, na hawezi tena kuongea. Taarifa za baadaye zilisema kwamba aliendelea katika hali hiyo ya kutoweza kuongea hadi alipoaga dunia, siku ya tano baadaye.
       Kumbe mimi ndiye niliyekuwa Kiongozi wa mwisho wa ngazi ya Taifa kuongea naye katika uhai wake! Kutokana na hali hiyo, ndiyo sababu mshituko wangu nilipopata taarifa ya kifo chake, ulikuwa ni mkubwa Zaidi.
      Hata hivyo nilifarijika nilipopewa heshima kubwa ya kuandika na baadaye kuusoma, wasifu (eulogy) wa marehemu Mwalimu Nyerere, katika mkusanyiko wa kitaifa wa maombolezo, uliofanyika kwenye uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam kabla mwili wake hujasafirishwa kwenda Butiama kwa mazishi.

Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu Julius Nyerere,
mahali pema peponi.