Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii

MAMLAKA ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASA) wameendelea na ukaguzi wa miundo mbinu ya maji inayohujumiwa na Wananchi wasio waaminifu.



Wananchi hao wamekuwa wanasababisha Mamlaka kupata hasara kubwa kwa kujiunganishia maji kwa njia ya wizi.

Zoezi la kuwabaini wahujumu wa miundo mbinu ya maji linaendelea kwa mikoa ya kihuduma DAWASA ambapo Mkoa wa Ubungo umeweza kubaini wizi wa maji kwa mteja asiye mwaminifu.

Akizungumzia zoezi hilo, Mwenyekiti wa kampeni maalum ya kupambana na wahujumu wa huduma na miundombinu Ubungo Frank Sulley amesema zoezi hilo limekua endelevu kwa Mkoa wa kihuduma Ubungo na wameweza kuwabaini wananchi wasio waaminifu wanaosababisha hasara kwa Mamlaka.

Amesema, wameweza kupata taarifa za kiintelijensia usiku wa kuamkia tarehe 27 Septemba 2019, na kufanikiwa kugundua wizi wa Maji eneo la Mbezi Inn alfajiri ya kuamkia tarehe 28 Septemba.

"Tuliweza kugundua hujuma iliyokua ikifanyika na Mteja asiye mwaminifu kwa kujaza maji kwenye kisima nyakati za usiku na na kuuza kwa Magari yanayofanya biashara ya kuuza maji,"amesema Sulley.

Amesema, ni kosa kisheria kwa mwananchi kujiunganishia maji na kuuza maji kwani hupunguzia Mamlaka Mapato na Serikali kwa ujumla.

Sulley ameeleza, mwananchi atakapokamatwa itapelekea kulipa faini isiyopungua milion 5 hadi milion 50 na ata kufikishwa Mahakamani.


Ofisi ya kihuduma Mkoa wa Ubungo inapenda kuwatahadharisha wananchi kuacha mara moja hujuma kwani hii ni hatari kwa ustawi wa Dawasa na Serikali kwa ujumla.
Mwenyekiti wa kampeni maalum ya kupambana na wahujumu wa huduma na miundombinu Mkoa wa Kihuduma Ubungo DAWASA, Frank Sulley akiwa na wafanyakazi wengine wa Mamlaka hiyo wakiendelea na zoezi la ukaguzi wa miundo mbinu na kubaini mwananchi akihujumu kwa kujaza maji kwenhe kisima na kuuza kwenye magari.
Mwenyekiti wa kampeni maalum ya kupambana na wahujumu wa huduma na miundombinu Mkoa wa Kihuduma Ubungo DAWASA, Frank Sulley akifungua kisima kinachodaiwa kujazwa maji na mwananchi na kisha kuyauza kwenye magari. Wakati wa ukaguzi wa miundo mbinu ya DAWASA ikiwa ni katika kupambana na wananchi wanaolihujumu Mamlaka.
Kisima kinachotumika na Mwananchi kujaza maji na kuyauza kwenye magari.