Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),Dkt Edwin Mhede akizungumza na Waandishi wa habari mkoani Mbeya leo,kuhusu mamlaka hiyo ilivyokusanya mapato jumla ya Shilingi Trilioni 1.7 katika kipindi cha mwezi Septemba 2019, ambayo ni sawa na asilimia 97 ya lengo la mwezi huo ambayo ni Trilioni 1.8 .
Baadhi ya Waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali wakimsikiliza Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),Dkt Edwin Mhede alipokuwa akizungumza nao leo mkoani Mbeya kuhusu mamlaka hiyo ilivyokusanya mapato yake yenye jumla ya Shilingi Trilioni 1.7 katika kipindi cha mwezi Septemba 2019, ambayo ni sawa na asilimia 97 ya lengo la mwezi huo ambayo ni Trilioni 1.8 .
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imekusanya mapato ya Serikali jumla ya TZS 1.767 trilioni katika kipindi cha mwezi Septemba 2019. Makusanyo haya, ambayo ni sawa na ufanisi wa 97.20% ya lengo letu la kukusanya jumla ya kiasi cha TZS 1.817 trilioni katika kipindi cha mwezi Septemba 2019, hayajawahi kutokea tangu kuanzishwa kwa TRA. Kwa kulinganisha na makusanyo ya mwezi Septemba 2018, makusanyo haya ya mwezi Septemba 2019 yamekua kwa wastani wa 29.18%.
Ufanisi huu wa mwezi Septemba 2019 ni mwendelezo wa ongezeko la makusanyo tangu mwaka wa fedha wa 2019/2020 ulipoaza mnamo mwezi Julai 2019. Hii ni kwa sababu katika kipindi cha mwezi Julai na Agosti 2019, TRA tulifanikiwa kukusanya kiasi cha TZS 1.256 trilioni (ambayo ilikuwa ni ufanisi wa 91.92% ya lengo la kukusanya TZS 1.367 trilioni) na TZS 1.335 trilioni (sawa na ufanisi wa 96.05% ya lengo la kukusanya TZS 1.409 trilioni), sawia. Aidha, makusanyo haya ni kiashiria kwamba Walipakodi na Watanzania walio wengi sasa wameelewa, wamekubali, na wameitikia wito wa Serikali ya Awamu ya Tano wa kuongeza mapato ya ndani kwa ajili ya maendeleo ya Taifa letu.
Hivyo, TRA inawashukuru walipakodi wote waliochangia makusanyo hayo kwa kulipa kodi zao kwa hiari. Pia, tunaishukuru Serikali (kwa ujumla wake) kwa kuendelea kuisaidia TRA katika kutekeleza majukumu yake ya kukusanya na kuhasibu mapato ya Serikali.
Kwa namna ya kipekee, tunapenda kuvishukuru vyombo vya habari kwa juhudi wanazofanya kuwahabarisha na kuelimisha umma juu ya ulipaji kodi. Aidha, tunapenda kuwahimiza wale wote ambao bado wanasuasua kujitokeza kulipa kodi hizo kwa wakati. Vile vile, tunaendelea kuwasisitiza walipakodi na wananchi wote ambao wana changamoto za kikodi kutembelea Ofisi za TRA na kuonana na Makamishna, Mameneja wa Mikoa, na Mameneja wa Wilaya kwa ufumbuzi wa changamoto hizo.
Pamoja na mafanikio haya, tunajua kuwa bado hatujafikia malengo yetu. Aidha, TRA tunatambua kuwa mafanikio haya yanakuja na changamoto. Ni lazima sote, kwa maana ya walipa kodi na Watendaji wa TRA, tukabiliane na changamoto hiyo na tuishinde. Kwa pamoja tunaweza kuishinda changamoto hiyo ambayo ni kuhakikisha uendelevu wa ufanisi huu mkubwa kwa miezi ijayo. Hivyo, nawatia moyo walipa kodi na Watumishi wenzangu kuwa bado tunayo kazi kubwa mbele yetu ya kuendelea kufanya vizuri zaidi na kuzidi.
Baadhi ya mikakati iliyopelekea kiasi hiki kikubwa cha ukusanyaji ni pamoja na kuziba mianya ya ukwepaji kodi kwa kusimamia kikamilifu Sheria za kodi, kuweka msisitizo wa matumizi ya mashine za kutolea risiti za kielektroniki (EFD receipts), elimu kwa mlipakodi, kuendelea kukujenga mifumo rafiki ya ukusanyaji kodi, na zoezi linaoendelea la kuboresha huduma kwa mlipakodi.
Wakati huo huo, Mamlaka inapenda kuwakumbusha wamiliki wote wa majengo nchini kujitokeza kulipia kodi za majengo haraka iwezekanavyo. Hii itawaepusha na usumbufu wa kulipa mwishoni mwa mwaka wa fedha 2019/2020 kwani kwa sasa viwango ni rafiki na vinalipika. Viwango hivyo kwa mwaka ni TZS 10,000 kwa nyumba ya kawaida, TZS 50,000 kwa kila sakafu nyumba ya ghorofa katika Majiji, Manispaa, na Halmashauri za Miji, na TZS 20,000 kwa jengo la ghorofa katika maeneo ya Halmashauri za Wilaya. Wamiliki wote wa majengo mnaweza kulipa kodi hii kwa njia ya simu za mkononi. Halikadhalika, Mameneja wa TRA katika Ofisi zetu za Mikoa na Wilaya wameweka utaratibu mzuri wa kumwezesha kila Mmiliki wa jengo kulipa kodi ya majengo kwa wakati.
Katika hatua nyingine, TRA inawaasa wale wote wanaojishughulisha na vitendo viovu vya kughushi risiti za kielektroniki za EFD. Tunatoa onyo kwamba muache mara moja tabia hiyo. Hii ni kwa sababu, kwa oparesheni tunayoendelea nayo ya kufuatilia matumizi sahihi ya EFD, kwa wataobainika watachukuliwa hatua kali za Kisheria ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani. Kila mwananchi na mfanyabiashara atambue wajibu wake uliopo kwa mujibu wa Sheria wa kudai risiti kwa kila manunuzi na kutoa risiti kwa kila mauzo.
Kwa sasa TRA imesogeza huduma karibu na walipakodi na wananchi kwa ujumla kwa kuwa sasa mnaweza kupiga simu bure kupitia namba 0800750075 au 0800780078 na kwa upande wa barua pepe tafadhali tuandikie huduma@tra.go.tz. Vile vile, mnaweza kutuma ujumbe kupita namba ya Whatsapp +255744233333.
Tunatanguliza shukrani zetu kwa ushirikiano mnaoendelea kuipatia TRA katika kutekeleza majukumu yetu.
“Pamoja Tunajenga Taifa Letu”
Imetolewa na:
Dr. Edwin P. Mhede, Ph.D.
KAMISHNA MKUU