Baadhi ya Wananfunzi wa Shule ya Sekondari ya Chief Sarwat ya Wilaya ya Mbulu Mkoani Manyara wakibeba viti na meza muda mfupi mara baada ya kukabidhiwa msaada huo na Benki ya NMB wenye thamani ya shilingi milioni tano shuleni hapo.
Wafanyakazi wa Benki ya NMB Kanda ya kati wakiangalia mashuka na wafanyakazi wa Hospitali ya Wilaya ya Kiteto Mkoani Manyara muda mfupi baada ya benki hiyo kukabidhi msaada wa vifaa tiba wenye thamani ya zaidi ya milioni tano hospitalini hapo.
Benki ya NMB imetoa msaada wa madawati 215 katika shule za sekondari Mahenge, Vigoi na Isongo zilizoko Wilayani Ulanga mkoa wa Morogoro na Ng’hoboko iliyoko Wilayani Meatu Mkoani Simiyu.
Mbali na hilo benki hiyo pia imetoa msaada wa vifaa tiba katika hospitali ya Wilaya ya Kiteto vyenya thamani ya shilingi milioni tano ambapo vifaa hivyo vilivyotolewa ni pamoja na vitanda na mashuka na magodoro.
Msaada huo wa madawati umegharimu kiasi cha sh. Milioni 20, ambapo katika shule za Wlaya ya ulanga benki hiyo imetoa madawati 165 yaliyogharimu Milioni 15 huku katika shule ya Ng’hoboko imetoa madawati 50 ambayo yamegharimu Milioni 5.
Vifaa hivyo pamoja na madawati vimetolewa kwa nyakati tofauti ndani ya wiki hii, ambapo vinaifanya benki hiyo kuchangia katika shughuli za maendeleo jumla ya shilingi Milioni 675 hadi sasa kwa mwaka huu tu.
Meneja wa benki hiyo kanda ya Magharibi Sospeter Magesse akiongea katika hafla ya kukabidhi madawati shule ya Ng’hoboko alisema kuwa msaada huo umetolewa ili kuwawezesha wanafunzi wasome vizuri.
Alisemakuwa benki hiyo imekuwa ikitenga kiasi cha sh. Bilioni moja kila mwaka kwa ajili ya kurejesha kwa wananchi, pesa ambayo imekuwa ikitumika kuboresha huduma za elimu, na afya.
“ NMB kama benki ya watanzania itaendelea kusaidiana na serikali pamoja na watanzania katika kuboresha huduma za afya na elimu, tuna imani kwa msaada huu wanafunzi watajisomea vizuri,” alisema Magesse.
Naye Nsolo Mlozi Meneja wa benki hiyo kanda ya kati akikabidhi vifaa tiba katika hospiali hiyo alisema kuwa NMB inatoa msaada huo kama njia ya kurudisha faida kwa wananchi ambao ndiyo wateja wao wakubwa.
“ Ingawa Serikali inafanya makubwa, Benki hiyo inao wajibu wa kuunga mkono juhudi hizo za maendeleo kwa kusaidia jamii kwani kupitia jamii hii hii, ndio imeifanya benki NMB kuwa hapa ilipo na kubwa kuliko benki yoyote hapa nchini,” Alisema Mlozi.
“ Vifaa hivi vya tiba na afya tunavyokabidhi leo ni moja ya ushiriki wetu katika maendeleo ya jamii na sisi kama benki inayoongoza Tanzania tunahakikisha jamii inayotuzunguka inafaidika kutokana na faida tunayoipata,” aliongeza Mlozi.
Mkuu wa Wilaya ya Ulanga Mkoani Morogoro Ngolo Malenya akipokea madawati ameishukuru benki ya NMB kwa kutoa madawati 165 kwa ajili ya wanafunzi wa shule za sekondari za mahenge ,vigoi na isongo
Ametoa wito kwa wanafunzi hao kuwa mabalozi kwa wazazi wao kwa kuwaeleza mambo mazuri yanayofanywa na benki hiyo ili pia wazazi hao waiunge mkono benki hiyo kwa kufungua account mbalimbali ili NMB izidi kurudisha faida wanazopata kwa jamii kwa kuleta maendeleo.
Naye Mkuu wa wilaya ya Meatu Dkt Joseph Chilongani aliishukuru benki ya NMB huku akitaka wanafunzi wa shule hiyo na walimu kuhakikisha madawati hayo yanatunzwa ili kudumu kwa muda mrefu.
“ Kuna haja ya kuweka adhabu kidogo kwa wale ambao watahusika kuaribu haya madawati, akiaribu mwanafunzi yeye au mzazi wake wahusike katika kutengeneza, tunataka haya madawati yatumiwe na wadogo zetu ili waone umuhimu wa NMB,” Alisema Chilongani.